Monday, September 3, 2018

pendekezo la utafiti


CHUO KIKUU CHA IRINGA

KITIVO CHA SAYANSI NA ELIMU
IDARA YA LUGHA NA MAWASILIANO.
JINA LA KOZI:                                          MBINU ZA UTAFITI NA UANDISHI WA TASNIFU    KATIKA LUGHA NA FASIHI
           
JINA LA MHADHIRI:                                CHALAMILA, A.
















SWALI: Andaa pendekezo la utafiti
MADA YA UTAFITI: KUCHUNGUZA KUDIDIMIA KWA KIWANGO CHA UFASAHA NA UKUAJI WA MATUMIZI YA LUGHA YA KISWAHILI KUTOKANA NA MATUMIZI YA REJESTA HUSUSANI YA KUGEUZA MAUMBO (KINYUME).
MAANA YA ISTILAHI MBALIMBALI
  1. Dereva – ni mwendeshaji wa vyombo vyenye mitambo hasa ya nchi kavu
  2. Kondakta- Mtu anayepokea nauli na kutoa tiketi katika gari ya abiria
  3. Geuza maumbo (kinyume)- Hii ina maana ya kitendo cha kugeuza neno kwa mfano abiria inakuwa aribia
  4. Haisi-  ni gari ndogo ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 12 hadi 20
  5. Kosta- ni gari ya saizi ya kati ya kubebea abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 25 hadi 40.










YALIYOMO
SURA YA KWANZA
1.0       Utangulizi.....................................................................................1
1.1 Historia ya Rejesta...........................................................................1
1.2 Tamko la Utafiti...............................................................................2
1.3  Kusudi la Utafiti..............................................................................2    
1.4  Malengo ya Utafiti...........................................................................2
1.5 Maswali ya Utafiti............................................................................2
1.6 Tatizo la Utafiti.................................................................................3
1.7 Umuhimu wa Utafiti.........................................................................3
1.8 Nadharia ...........................................................................................4
   1.8.1 Nadharia ya Utabia.....................................................................4
   1.8.2 Nadharia ya Umaanishaji...........................................................5
1.9 Changamoto za Utafiti.....................................................................6
SURA YA PILI             
2.0       Mapitio ya Vitabu..........................................................................7
2.0     Pengo la Utafiti..............................................................................8
SURA YA TATU
3.0   Mbinu za Utafiti...............................................................................9
3.1   Hojaji...................................................................................9
3.2    Mahojiano...........................................................................9
3.3    Kushiriki.............................................................................9
3.1 Eneo la Utafiti.................................................................................10
3.2 Zana za Utafiti.................................................................................10
3.3 Uteuzi wa Sampuli...........................................................................10
3.4 Uchambuzi wa Data.........................................................................11
4.0 Hitimisho........................................................................................12


SURA YA KWANZA
1.0 Utangulizi
Kutokana na uchunguzi unaofanywa mara kwa mara na wataalamu wa maswala ya matumizi ya lugha miongoni wa wazungumzaji wa lugha ya kiswahili, ni bayana kuwa pana athari kubwa katika lugha ya kiswahi. Ili madereva au makondakta   wahisi kuwa ni sehemu katika jumuiya ya  wenzao , aghalabu huishia kujiingiza katika matumizi ya rejesta kwa jino na ukucha katika mawasiliano yao ya kila siku.       
Madereva   na makondakta hususani gari ndogo za abiria kama haisi na kosta ndio ambao wamegeuka kuwa lindi la matumizi ya mtindo huu wa lugha. Baadhi ya dereva na kondakta huishia kuzama kabisa katika lindi la matumizi ya rejesta na kupoteza umilisi wao wa lugha ya Kiswahili. Kufua dafu kwao katika matumizi ya rejesta kwa asilimia kubwa hutegemea mawasiliano tofauti, wanaotagusana na sababu nyinginezo.
Mawasiliano pia kwa upande wake hutegemea lugha kama chombo chake cha kufinyanga na kuwasilisha mawazo, hisia, na maelezo kwa njia na utaratibu fulani. Mwasilishaji wa ujumbe anapoanza kuzama katika matumizi ya rejesta katika mawasiliano yake, yapo madhara makubwa na changamoto ambazo yeye hupitia baina yake na watumiaji wengine wa lugha ya Kiswahili hasa abiria wanakuwa kwenye gari hiyo kwani wanakuwa hawajui chochote kinachoongelewa na wawili hawa yaani dereva na kondakta wake.
Lengo kuu la utafiti huu litakuwa kuchunguza suala la kudidimia kwa kiwango cha ufasaha na ukuaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kutokana na matumizi ya rejesta katika maneno ya kiswahili mfano badala ya kusema Twende anasema Ndetwe. Makala haya itatoa kauli kwamba matumizi rejesta yameathiri sana matumizi na hadhi ya lugha ya Kiswahili. Kutokana na mambo haya yote, utafiti huu unalenga kukusanya data itakayoniwezesha kuratibu, kuchanganua na kuwasilisha matokeo ya athari ya matumizi ya rejesta katika lugha ya Kiswahili.
1.1 Historia ya Rejesta.        
Rejesta au sajili ni mtindo wa lugha unaotumiwa na watu kulingana ma mazingira au kazi wanayofanya lengo huwa ni kutaka waelewane wao kwa wao na pengine kuwatenga watu wengine. Katika mukhtadha huo ni sawa kusema kuwa rejesta ni mtindo wa lugha ambao katika matumizi yake haufuati mfumo rasmi wa sarufi kwani watu hubuni namna ya kuwalisha taarifa kwa namna wanavyofikiria kwani rejesta hizi wakati mwingine huhusisha kugeuza maumbo ya maneno (kinyume) kwa mfano anasema tasko jakunai badala ya kusema kosta inakuja. Jina hili limepewa msimbo wa kinyume kwani huhusisha ugeuzaji wa maneno. Rejesta ni mtindo wa lugha uliaonza kutokana na sababu mbalimbali kwa  mfano  ubinafsi, maingiliano, kupita kwa wakati, shughuli iliyopo,tofauti za hadhi za wahusika (uhusiano wa wahusika),matumizi ya uficho/tafsida. Kutoka na kuwepo kwa mambo haya ndiko kulikopelekea kuwepo kwa mtindo huu wa lugha unaoitwa rejesta Nkwera, (2003).
1.2 Tamko la Utafiti
Utafiti huu utahusisha zaidi kudidimia kwa ufasaha na ubora wa lugha ya Kiswahili kutokana na matumizi makubwa ya rejesta ambazo hukiuka kaida za lugha katika viwango vyote vinne ambavyo ni fonolojia, mofolojia, semantiki na sintaksia lengo kubwa ni kutaka kuufahamisha uma hasa madereva na makondakta ambao wameingia katika wimbi hili ili watambue kwa kiasi gani wanadidimiza ufasaha na ubora wa lugha ya Kiswahili kama lugha ya taifa.
1.3 Kusudi la Utafiti
Lengo kuu la utafiti huu litakuwa kuchunguza suala la kudidimia kwa kiwango cha ufasaha na ukuaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kutokana na matumizi ya rejesta hususani ya kugeuza maumbo (kinyume).
1.4 Malengo ya Utafiti.
(i)     Kufahamisha dereva na kondakta wake kuhusu madhara ya rejesta katika kudidimia kwa ufasaha wao katika lugha ya Kiswahili.
(ii)   Kuelimisha dereva, kondakta pamoja na watu wengine waelewe athari mbaya itokanayo na kutotumia lugha sanifu ya Kiswahili katika mawasiliano.
(iii) Kubaini namna kundi wakilishi linatumia rejesta hususani zinazohusu watu katika mawasiliano
1.5  Maswal ya Utafiti (Nadharia Tete)
(i)     Rejesta ni nini?
(ii)   Nini chanzo rejesta?
(iii) Kuna faida gani kutumia rejesta katika mawasiliano?
(iv)  Kuna athari zozote katika lugha ya kiswahili kutokana na matumizi ya rejesta? Zitaje
(v)   Je watu rika ipi wanaopenda kutumia rejesta? Kwanini?
(vi)  Kwa kiwango kipi kundi lengwa hutumia rejesta katika mawasiliano?
(vii)           Je ulishawahi kuona rejesta zinazohusisha ugeuzaji wa maneno kwa  mfano anajaku
(viii)         Unafikiri kwanini rejesta hizi zinapelekea kupotea kwa maneno ya lugha ya kiswahili?
1.6 Tatizo la Utafiti                                                                                          
Mtindo wa rejesta kama mitindo mingine ya lugha imeathiri sana lugha ya kiswahili. Matumizi yake yameathiri kwa njia moja ama nyingine namna watu wanavyokitumia Kiswahili katika mawasiliano na maandishi. Athari hizi zaweza kuwa chanya au hasi kutegemea:
·         Mazingira ya mawasiliano
·         Madhumuni ya ujumbe husika
·         Hekima ya utafsiri alio nao mlengwa wa ujumbe
·         Kiwango cha uhusiano
·         Umri wa watumiaji wa mtindo kinyume
·         Miongoni mwa nyingine nyingi.
Kutokana na hili, utafiti huu utasaidia kutathmini jinsi rejesta hususani zinazohusu watu zinavyoathiri  lugha ya Kiswahili.
1.7  Umuhimu wa Utafiti.
Kuna haja ya kufanya utafiti zaidi kuhusu athari za matumizi ya rejesta katika lugha ya Kiswahili. Utafiti huu utasaidia kukusanya data na kuzihifadhi katika maandishi, kwani mambo mengi ya rejesta hususani matumizi ya maneno kinyume kwa mfano badala ya basi inakuwa siba, kwani bado yamehifadhiwa vichwani mwa watu tangu yalipoanzishwa. Utunzaji wa kumbukumbu wa namna hii siyo thabiti, kwani wakati wowote data hizo huweza kupotea au kusahaulika kutokana na maradhi au kifo.
Utafiti huu una umuhimu mkubwa sana kwa Taifa kwani utasaidia kufafanua naamna rejeta inavyodidimiza ufasaha wa lugha ya kiswahili na namna taaluma hii inavyozidi kukiuka kanuni au kaida ambazo mzungumzaji yeyote wa lugha ya Kiswahili anapaswa kuzingatia.      
Pia utafiti huu utasaidia watu watakao soma matini hii kubadilika kimtazamo na hivyo kuamsha ari ya kudadisi zaidi mambo mbalimbali ya Kiswahili hususani athari za matumizi ya mitindo mbalimbali katika lugha ya kiswahili. Pia utafiti huu utasaidia wanafunzi mbalimbali katika kutumia kama rejea za tafiti zao.
Vilevile utasaidia kuonesha/kuelewa jinsi lugha ya Kiswahili inavyopitia matatizo mengi katika kupiga hatua zake za kuwa lugha ya kimataifa na masiala mbalimbali yanayozuia Kiswahili kukua haraka kama lugha zingine za kimataifa.
1.8 Nadharia
1.8.1 Nadharia ya Utabia
Msingi wa utafiti huu kinadharia, utaegemea dhana ya Nadharia Ya Utabia.Nadharia hii ilitumika Marekani kati ya 1950-1960. Ina misingi yake katika nadharia ya kisaikolojia ya utabia.Katika saikolojia, waaasisi wa utabia walilenga kueleza namna tabia inavyojengwa. Waliamini kuwa tabia ilijengwa tu ikiwa itarudiwa na kutunzwa. Tabia isiyorudiwa hufifia.
Waliamini kuwa jambo analofunzwa mtu mwanzo linaathiri lile analojifunza baadaye.Kutokana na maoni hayo, tunafahamu kuwa ujifunzaji wa lugha ya pili ni sawa na ujifunzaji wa tabia yoyote ile kama vile kukimbia. Nadharia hii inamsaidia mtafiti kuchunguza kiwango cha madhara ya mtumiaji wa lugha ya Kiswahili kutokana na mazoea ya kutumia rejesta.
Waasisi wa lugha hii wanasisitiza yafuatayo:
·         Kukariri na kurudiarudia matamshi mazuri ya vipande vya mazungumzo hukuza lugha hiyo.
·         Kutofanya makosa ya kisarufi ili kujenga tabia ya matumizi ya lugha kwa ufasaha.
·         Vipengele vya lugha hufundishwa kwa njia ya kusikiliza na kuzungumza kasha maandishi huja baadaye.
·         Miundo ya kisarufi ya lugha ifundishwe kupitia ukariri wa makala kama tamthiliya.
·         Katika ufundishaji wa sarufi, wanafunzi wakariri na kuiga vipengele hivi ili wazoee na baadaye wang’amue wenyewe kwa kukisia kanuni zinazotawala lugha. Kwa mfano, kurudia umoja na wingi wa nomino za ngeli fulani na baadaye kupewa nomino katika umoja watambue wingi wake.
Hivyo waasisi wa nadharia hii walichunguza jinsi mtu anavyojifunza lugha kutokana na mazoea.Hivyo nadharia hii ilimsaidia mtafiti katika kuchunguza jinsi mazoea ya matumizi ya geuza maumbo yanavyoathiri Kiwango cha uelewa na ufasaha wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa watumizi wake kimawasiliano na hata kimaandishi.
Nadharia hii inamsaidia mtafiti kufahamu jinsi mazoea katika matumizi ya geuza maumbo au lugha yoyote ile yanavyoathiri kiwango cha umilisi wa lugha ya kwanza au Kiswahili. Matumizi ya geuza maumbo husababisha kudidimia kwa  ubora wa mtumiaji wa Kiswahili katita viwango vya sarufi na kuogeza makosa ya kisarufi katika viwango vyote vinne ambavyo ni maumbo, maana, matamshi na muundo wa uandishi. Pia mazoea ya kuzungumza geuza maumbo huchangia kudidimia kwa msamiati wa lugha ya Kiswahili kwa watumiaji wake.
Kwa wale ambao wanajifunza lugha ya kwanza ambayo ni Kiswahili kwao wataathirika sana na lugha ya geuza maumbo kutokana na kuwepo kwa mazingira ambayo watu wengine wanatumia lugha ya geuza maumbo. Jambo hili litachangia yeye kujifunza lugha ya Kiswahili iliyojaa kasoro za kisarufi, kimantiki na isiyo sanifu.           
1.8.2 Nadharia ya umaanishaji
Nadharia nyingine itakayofaa katika utafiti mzima ni ile ya Umaanishaji iliyoasisiwa na Grice (1975). Nadharia hii inaelezea kwamba kuwa watu huwa hawasemi mambo waziwazi; na ili kupata ujumbe kamilifu kutokana na kile wakisemacho, ni sharti kuwe na umaanishaji katika maana. Kauli hii imejengwa kwa msingi kuwa wasemaji humaanisha mambo yanayozidi walichokisema na la muhimu katika kujifunza lugha ni mawasiliano.        
Kwa jumla, nadharia hii inashikilia dhana kuwa maana ya jambo, matukio au hali fulani hutokana na tafsiri ya kimuktadha pamoja na elimu shirikishi. Yaani, maana ni zao la ushirikiano baina ya msikilizaji na msemaji kwa kuzingatia kaida nne: kanuni ya idadi, namna, uhusiano, na ukweli. Nadharia hii inatusaidia kufahamu kuwa jambo la muhimu katika lugha fulani ni maana ya maneno yanayotumika.Ikiwa lugha ya geuza maumbo itaendelea kutumika, kiwango cha ulewa katika mawasiliano kitadidimia kwa kuwa si watu waote wanaotumia lugha ya Kiswahili wanaelewa maana ya maneno yanayotumiwa katika lugha ya geuza maumbo.
Nadharia hii inatuonyesha jinsi umuhimu wa maana katika matumizi ya lugha ulivyo na nguvu kupiku maneno yenyenyewe. Geuza maumbo imechangia kubadilika kwa maana ya maneno ya Kiswahili na kupewa maana nyingine ambayo watumizi wa Kiswahili hawafahamu. Jambo hili limechangia kupotoka kwa maana ya maneno ya Kiswahili na kudidimia kwa kiwango cha hadhi ya Kiswahili kwa kuwa watumizi wake wamelazimika kuelewa maana fiche ya maneno ya Kiswahili kama jinsi maneno hayo yanavyomanisha katika lugha ya geuza maumbo.
1.9 Changamoto za Utafiti
Upungufu wa rejea na muda kutokuwa wa kutosha ni changamoto mojawapo utakaoukabili utafiti huu. Si hivyo tu, vilevile upungufu wa fedha, kutokupata ushirikiano kwa baadhi ya watafitiwa.








SURA YA PILI
2.0 Mapitio ya Vitabu                                        
Ili kuweza kujua madhara ya rejesta katika lugha ya Kiswahili, mtafiti asome makala na vitabu vilivyoandikwa na wataalamu mbalimbali wa lugha kama inavyooneshwa katika sura hii;
Matumizi ya lugha kwa maana nyingine iliyo finyu, ni Rejesta. Rejesta ni mtindo wa lugha inayotumika mahali penye shughuli fulani ambayo ni tofauti na lugha ya kawaida. Kwa mfano, lugh ya wavuvi, washairi, ya kibiashara, ya kihuni, n.k. Kwa upande mwingine kuna rejesta zinazotokana na umri, kwa mfano vijana wana rejesta yao, wazee wana yao, wanawake wana yao, marafiki nao wana rejesta yao, rejesta ya mitaani, nk.
Rejesta: Halliday (1989), anafasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi au shughuli. Vilevile fasili hii inaendana na fasili ya Habwe na Karanja (2007). Kwa ujumla tunaweza kufasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi fulani, muktadha wa matumizi, lengo na uhusiano wa wanaowasiliana. Katika muktadha rasmi rejesta hurejelea upande mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi, adabu maalum na matumizi ya lugha fasaha, mfano katika elimu, mahakamani nakadhalika. Pia Rejista ni matumizi ya lugha kulingana na muktadha maalum. Miktadha tofauti husababisha aina mbalimbali za lugha. Baadhi ya vipengele vya miktadha hiyo ni mada, eneo la matumizi ya lugha, mahusiano baina ya wahusika, umri, jinsia, wakati, na kadhalika, mifano ya rejesta katika lugha ni Mifano ya rejista za lugha ni: lugha ya mazungumzo, lugha ya sheria, lugha ya biashara, lugha ya sayansi, na lugha ya dini Massamba,  (2004).
Rejesta, Kwa ujumla tunaweza kufasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi fulani, muktadha wa matumizi, lengo na uhusiano wa wanaowasiliana. Katika muktadha rasmi rejesta hurejelea upande mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi, adabu maalum na matumizi ya lugha fasaha, mfano katika elimu, mahakamani na kadhalika lengo kubwa huwa ni kutambulisha jamii husika. Kutokana fasihili imepelekea kuwepo kwa aina mbalimbali za rejesta kama rejesta za mitaani, rejesta za mahali na rejesta zinazohusu watu. Buliba, Aswani, Kimani Njogu & Alice Mwihaki, (2006)
2.1 Pengo la Utafiti.
Kutokana na mapitio hayo ya tafiti mbalimbali mtafiti ameona kwamba tafiti nyingi zimeelezea kuhusu kuchipuka na kukua kwa rejesta , lakini kati ya tafiti hizo hakuna tafiti zozote zilizoelezea kuhusu namna ya matumizi ya rejesta hususani zinazo wahusu watu katika kipengele cha kugeuza maumbo ya maneno kinavyo didimiza na kuathiri  lugha ya Kiswahili. Hivyo basi, utafiti huu utakusudia kuziba pengo hilo.














SURA YA TATU
3.0 Mbinu za Utafiti
Katika utafiti huu mtafiti atatumia mbinu mbalimbali ambazo zitamwezesha kukusanya data anazozihitaji katika utafiti wake. Mbinu hizo ni kama vile;
3.1 Hojaji.
Mtafiti ataitumia mbinu hii ili kuweza kupata data mbalimbali zilizohusu matumizi ya lugha ya geuza maumbo. Baadhi ya maswali mtafiti atakayouliza yatakuwa kama ifuatavyo;
(i)     Je wanaifahamu rejesta  ya geuza maumbo (kinyume)?
(ii)   Je wanatumia rejesta ya geuza maumbo (kinyume) kwa dhamira gani katika mawasiliano?
(iii) Je wanapendelea lugha ipi baina ya geuza maumbo (kinyume) na Kiswaahili inayofanikisha mawasiliano haraka?
(iv) Je dhamira zinazopatikana katika matumizi ya geuza maumbo (kinyume) ni tofauti na zile zinazopatikana katika matumizi ya lugha ya Kiswahili?
(v)   Wanahisi matatizo yoyote yale kwa kuwepo kwa lugha ya geuza maumbo (kinyume)?
3.2 Mahojiano.
Mtafiti atawahoji watu mbalimbali kuhusu uelewa wao wa rejesta ya geuza maumbo (kinyume) pamoja na Kiswahili na kuwaomba wachangie maoni yao kuhusu ikiwa yapo matatizo yanayotokana na kuongezeka kwa matumizi ya rejesta ya geuza maumbo (kinyume) kwa lugha ya Kiswahili. Pia atawaomba wahojiwa waweze kujieleza kwa Kiswahili sanifu kwa mda mfupi na walinganishe mazungumzo yao ya sasa na yale ya kabla ya wao kujifunza rejesta ya geuza maumbo (kinyume).
3.3 Kushiriki.
Mtafiti atashiriki mazungumzo baina yake na watu wa umri mbalimbali katika  maeneo yao ya kazi kwa kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha kuu ya mawasiliano. Pia atashiriki katika soga za watu mbalimbali wanaotumia rejesta ya geuza maumbo.
3.1 Eneo la utafiti
Mtafiti atafanya utafiti wake katika eneo la Manispaa ya Iringa katika mkoa wa Iringa.
3.2  Zana za Utafiti za Kukusanya Data
Mtafiti atatumia vifaa kama vile kalamu na karatasi katika kuandika data mbalimbali atakazozipata katika utafiti wake. Pia atatumia:
-        kinasa sauti.
-        kamera ya picha tuli.
-        kamera ya video ili kurekodi mahojiano na majadiliano yote.
Mtafiti atahitajika kusikiliza kwa makini na kuandika katika karatasi maneno na masuala yatakayojitokeza wakati wa majadiliano baina yake na watumizi wa lugha ya geuza maumbo na Kiswahili.
3.3 Uteuzi wa Sampuli
Sampuli ya watafitiwa isichaguliwe kiholela bali izingatie vigezo vifuatavyo; umri na maeneo ya kazi ili kupata wawakilishi sahihi. Vilevile uteuzi utazingatia umahiri wa wazungumzaji katika kutumia rejesta ya geuza maumbo (kinyume) na Kiswahili. Ingawa sampuli itazingatia umri, maeneo ya kazi na umahiri wa lugha, lakini watu wenye umri wa kati wapewa umuhimu mkubwa kutokana na uzoefu wao wa maisha na kuaminika kwao kuwa wanaujuzi mkubwa wa lugha husuka, pia kutokana na kutumia mtindo huu kwa muda mrefu inasadikika kuwa wameshiriki katika matukio mbalimbali na hivyo kuweza kujua vizuri zaidi dhima na dhamira ya lugha ya Kiswahili. Hivyo basi mtafiti atachagua sampuli ya takribani watu 122 ambao ni dereva na kondakta wanaofanya shughuli ya kuendesha magari madogo aina ya haisi na kosta katika Manispaa ya Iringa.
Watafitiwa hawa washiriki katika utafiti wa madhara ya rejesta ya  geuza maumbo (kinyume) katika lugha ya Kiswahili. Mchango wa sampuli hiyo uwe kama ufuatao; Katika mchanganuo huo, watu wa rika, Dereva na Kondakta  waonyeshwe kwa kutumia jedwali.         
Umri
Dereva
Kondakta
20-24
7
15
25-29
30
10
30-34
20
10
35-39
15
5
40-44
10
0
JUMLA
82
40

3.4 Uchambuzi wa Data
Mtafiti achunguze na kuchambua data alizokusanya ili ziweze kutumika katika utafiti wake. Ili kupata usahihi katika data mbalimbali atazokusanya, mtafiti alinganishe na kuzichuja data hizo.
Vilevile kutokana na data atakazozikusanya mtafiti, vijana wa umri wa miaka 35-49  watakuwa na ufasaha katika kutumia lugha ya Kiswahili kuliko vijana wa umri wa miaka 20-34 hasa kutokana na madhara finyu ya geuza maumbo kwao ikilinganishwa na jinsi vijana walivyoadhiriwa na lugha ya geuza maumbo.
Aidha, mtafiti ayagawaanye madhara ya geuza maumbo kwa lugha ya Kiswahili katika kategoria mbili:
(i)     Umri.
(ii)   Maeneo ya makaazi.



4.0 Hitimisho
Utafiti huu utahusu madhara ya rejesta katika kudidimia kwa ufasaha wa lugha ya Kiswahili. Kutokana na uchambuzi wa data, utafiti utatoa matokeo yanayoonesha kwamba rejesta ina madhara mbalimbali kama vile: madhara ya kisarufi, madhara ya kimsamiati, madhara ya kiufasaha na umilisi wa Kiswahili, madhara ya umoja na mshikamano katika jamii.
Kutokana na utafiti huu wa madhara ya rejesta katika lugha ya Kiswahili yataonekana wazi kuwa matumizi ya rejesta bado yanaendelea kukiathiri Kiswahili kwa kiwango kikubwa hasa tukirejelea kuwa Kiswahili ni lugha ya taifa nchini Tanzania. Kiswahili ni lugha inayowapatanisha Watanzania.
Mtindo wa rejesta umeathiri uhusiano uliokuwepo kati ya madereva, makondakta na abiria kutokana na kuwa abiria wote wanatumia lugha moja kuu ya Kiswahili inayowaunganisha. Kutokana na kuzuka kwa rejesta hasa ya kugeuza maumbo (kinyume) baina ya madereva na makondakta, wasioelewa lugha hii hata kama wanaufahamu mzuri wa Kiswahili wanabanwa nje na wale wanaotumia mtindo huu wa lugha ya rejesta inayohusisha ugeuzaji wa maneno kwa mfano aribia akiwa na maana ya abiria katika mawasiliano yao.
Lengo kuu la utafiti huu litakuwa kuchunguza suala la kudidimia kwa kiwango cha ufasaha na ukuaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kutokana na matumizi ya rejesta hususani ya kugeuza maumbo (kinyume). Makala haya yatatoa kauli kwamba matumizi ya rejesta hii inavyoathiri sana matumizi na hadhi ya lugha ya Kiswahili. Kutokana na mambo haya yote,utafiti huu unalenga kukusanya data itakayoniwezesha kuratibu, kuchanganua na kuwasilisha matokeo ya athari ya matumizi ya rejesta katika lugha ya Kiswahili.





MAREJELEO
Buliba,  Aswani, Kimani Njogu & Alice Mwihaki. (2006). "Isimujamii kwa Wanafunzi wa Kiswahili", Nairobi: The Jomo Kenyatta Foundation
Halliday M.A.K (1989). Spoken and written language.UK:  Oxford university press.  
Massamba, D.  (2004), "Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Nkwera, Fr. F. V. (2003), Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu, Sekondari na Vyuo. Creative Prints Ltd: Dar es Salaam.



No comments:

Post a Comment