Monday, September 3, 2018
pendekezo la utafiti
CHUO
KIKUU CHA IRINGA
KITIVO CHA SAYANSI
NA ELIMU
IDARA
YA LUGHA NA MAWASILIANO.
JINA LA KOZI: MBINU ZA UTAFITI NA UANDISHI WA TASNIFU KATIKA LUGHA NA FASIHI
JINA LA MHADHIRI: CHALAMILA, A.
SWALI:
Andaa pendekezo la utafiti
MADA
YA UTAFITI: KUCHUNGUZA KUDIDIMIA KWA
KIWANGO CHA UFASAHA NA UKUAJI WA MATUMIZI YA LUGHA YA KISWAHILI KUTOKANA NA
MATUMIZI YA REJESTA HUSUSANI YA KUGEUZA MAUMBO (KINYUME).
MAANA
YA ISTILAHI MBALIMBALI
- Dereva – ni mwendeshaji wa vyombo vyenye mitambo hasa ya nchi kavu
- Kondakta- Mtu anayepokea nauli na kutoa tiketi katika gari ya abiria
- Geuza maumbo (kinyume)- Hii ina maana ya kitendo cha kugeuza neno kwa mfano abiria inakuwa aribia
- Haisi- ni gari ndogo ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 12 hadi 20
- Kosta- ni gari ya saizi ya kati ya kubebea abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 25 hadi 40.
YALIYOMO
SURA YA KWANZA
1.0
Utangulizi.....................................................................................1
1.1 Historia ya Rejesta...........................................................................1
1.2 Tamko la Utafiti...............................................................................2
1.3 Kusudi la
Utafiti..............................................................................2
1.4 Malengo ya Utafiti...........................................................................2
1.5 Maswali ya Utafiti............................................................................2
1.6 Tatizo la Utafiti.................................................................................3
1.7 Umuhimu wa Utafiti.........................................................................3
1.8 Nadharia ...........................................................................................4
1.8.1 Nadharia ya Utabia.....................................................................4
1.8.2 Nadharia ya Umaanishaji...........................................................5
1.9 Changamoto za Utafiti.....................................................................6
SURA YA PILI
2.0
Mapitio ya Vitabu..........................................................................7
2.0
Pengo la Utafiti..............................................................................8
SURA YA TATU
3.0
Mbinu za Utafiti...............................................................................9
3.1
Hojaji...................................................................................9
3.2
Mahojiano...........................................................................9
3.3
Kushiriki.............................................................................9
3.1 Eneo la Utafiti.................................................................................10
3.2 Zana za Utafiti.................................................................................10
3.3 Uteuzi wa Sampuli...........................................................................10
3.4 Uchambuzi wa Data.........................................................................11
4.0 Hitimisho........................................................................................12
SURA
YA KWANZA
1.0
Utangulizi
Kutokana na uchunguzi unaofanywa mara
kwa mara na wataalamu wa maswala ya matumizi ya lugha miongoni wa wazungumzaji
wa lugha ya kiswahili, ni bayana kuwa pana athari kubwa katika lugha ya
kiswahi. Ili madereva au makondakta wahisi kuwa ni sehemu katika jumuiya ya wenzao , aghalabu huishia kujiingiza katika
matumizi ya rejesta kwa jino na ukucha katika mawasiliano yao ya kila siku.
Madereva na makondakta hususani gari ndogo za abiria
kama haisi na kosta ndio ambao wamegeuka kuwa lindi la matumizi ya mtindo huu
wa lugha. Baadhi ya dereva na kondakta huishia kuzama kabisa katika lindi la
matumizi ya rejesta na kupoteza umilisi wao wa lugha ya Kiswahili. Kufua dafu
kwao katika matumizi ya rejesta kwa asilimia kubwa hutegemea mawasiliano
tofauti, wanaotagusana na sababu nyinginezo.
Mawasiliano pia kwa upande wake hutegemea
lugha kama chombo chake cha kufinyanga na kuwasilisha mawazo, hisia, na maelezo
kwa njia na utaratibu fulani. Mwasilishaji wa ujumbe anapoanza kuzama katika
matumizi ya rejesta katika mawasiliano yake, yapo madhara makubwa na changamoto
ambazo yeye hupitia baina yake na watumiaji wengine wa lugha ya Kiswahili hasa
abiria wanakuwa kwenye gari hiyo kwani wanakuwa hawajui chochote
kinachoongelewa na wawili hawa yaani dereva na kondakta wake.
Lengo kuu la utafiti huu litakuwa kuchunguza suala la
kudidimia kwa kiwango cha ufasaha na ukuaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili
kutokana na matumizi ya rejesta katika maneno ya kiswahili mfano badala ya
kusema Twende anasema Ndetwe. Makala haya itatoa kauli kwamba matumizi rejesta
yameathiri sana matumizi na hadhi ya lugha ya Kiswahili. Kutokana na mambo haya yote, utafiti huu unalenga
kukusanya data itakayoniwezesha kuratibu, kuchanganua na kuwasilisha matokeo ya
athari ya matumizi ya rejesta katika lugha ya Kiswahili.
1.1
Historia ya Rejesta.
Rejesta au sajili ni mtindo wa lugha unaotumiwa na watu
kulingana ma mazingira au kazi wanayofanya lengo huwa ni kutaka waelewane wao
kwa wao na pengine kuwatenga watu wengine. Katika mukhtadha huo ni sawa kusema
kuwa rejesta ni mtindo wa lugha ambao katika matumizi yake haufuati mfumo rasmi
wa sarufi kwani watu hubuni namna ya kuwalisha taarifa kwa namna wanavyofikiria
kwani rejesta hizi wakati mwingine huhusisha kugeuza maumbo ya maneno (kinyume)
kwa mfano anasema tasko jakunai badala
ya kusema kosta inakuja. Jina hili limepewa
msimbo wa kinyume kwani huhusisha ugeuzaji wa maneno. Rejesta ni mtindo wa lugha uliaonza kutokana na sababu
mbalimbali kwa mfano ubinafsi, maingiliano,
kupita kwa wakati, shughuli iliyopo,tofauti
za hadhi za wahusika (uhusiano wa wahusika),matumizi ya uficho/tafsida.
Kutoka na kuwepo kwa mambo haya ndiko kulikopelekea kuwepo kwa mtindo huu wa
lugha unaoitwa rejesta Nkwera, (2003).
1.2 Tamko la Utafiti
Utafiti
huu utahusisha zaidi kudidimia kwa ufasaha na ubora wa lugha ya Kiswahili
kutokana na matumizi makubwa ya rejesta ambazo hukiuka kaida za lugha katika
viwango vyote vinne ambavyo ni fonolojia, mofolojia, semantiki na sintaksia lengo
kubwa ni kutaka kuufahamisha uma hasa madereva na makondakta ambao wameingia
katika wimbi hili ili watambue kwa kiasi gani wanadidimiza ufasaha na ubora wa
lugha ya Kiswahili kama lugha ya taifa.
1.3 Kusudi la Utafiti
Lengo kuu la utafiti huu litakuwa kuchunguza suala la
kudidimia kwa kiwango cha ufasaha na ukuaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili
kutokana na matumizi ya rejesta hususani ya kugeuza maumbo (kinyume).
1.4 Malengo ya
Utafiti.
(i)
Kufahamisha dereva na
kondakta wake kuhusu madhara ya rejesta katika kudidimia kwa ufasaha wao katika
lugha ya Kiswahili.
(ii)
Kuelimisha dereva, kondakta
pamoja na watu wengine waelewe athari mbaya itokanayo na kutotumia lugha sanifu
ya Kiswahili katika mawasiliano.
(iii) Kubaini namna kundi wakilishi linatumia rejesta hususani zinazohusu watu
katika mawasiliano
1.5 Maswal ya Utafiti
(Nadharia Tete)
(i)
Rejesta ni nini?
(ii)
Nini chanzo rejesta?
(iii) Kuna faida gani
kutumia rejesta katika mawasiliano?
(iv) Kuna athari zozote katika lugha ya kiswahili
kutokana na matumizi ya rejesta? Zitaje
(v)
Je watu rika ipi wanaopenda kutumia
rejesta? Kwanini?
(vi) Kwa kiwango kipi kundi lengwa hutumia rejesta
katika mawasiliano?
(vii)
Je ulishawahi kuona rejesta
zinazohusisha ugeuzaji wa maneno kwa
mfano anajaku
(viii)
Unafikiri kwanini rejesta hizi
zinapelekea kupotea kwa maneno ya lugha ya kiswahili?
1.6 Tatizo la Utafiti
Mtindo wa rejesta kama mitindo mingine
ya lugha imeathiri sana lugha ya kiswahili. Matumizi yake yameathiri kwa
njia moja ama nyingine namna watu wanavyokitumia Kiswahili katika mawasiliano
na maandishi. Athari hizi zaweza kuwa chanya au hasi
kutegemea:
·
Mazingira ya
mawasiliano
·
Madhumuni ya ujumbe
husika
·
Hekima ya utafsiri alio
nao mlengwa wa ujumbe
·
Kiwango cha uhusiano
·
Umri wa watumiaji wa
mtindo kinyume
·
Miongoni mwa nyingine
nyingi.
Kutokana na hili, utafiti huu utasaidia kutathmini jinsi rejesta hususani
zinazohusu watu zinavyoathiri lugha ya
Kiswahili.
1.7 Umuhimu wa Utafiti.
Kuna haja ya
kufanya utafiti zaidi kuhusu athari za matumizi ya rejesta katika lugha ya
Kiswahili. Utafiti huu utasaidia kukusanya data na kuzihifadhi katika
maandishi, kwani mambo mengi ya rejesta hususani matumizi ya maneno kinyume kwa
mfano badala ya basi inakuwa siba, kwani bado yamehifadhiwa vichwani
mwa watu tangu yalipoanzishwa. Utunzaji wa kumbukumbu wa namna hii siyo
thabiti, kwani wakati wowote data hizo huweza kupotea au kusahaulika kutokana
na maradhi au kifo.
Utafiti huu una
umuhimu mkubwa sana kwa Taifa kwani utasaidia kufafanua naamna rejeta
inavyodidimiza ufasaha wa lugha ya kiswahili na namna taaluma hii inavyozidi
kukiuka kanuni au kaida ambazo mzungumzaji yeyote wa lugha ya Kiswahili
anapaswa kuzingatia.
Pia utafiti huu
utasaidia watu watakao soma matini hii kubadilika kimtazamo na hivyo kuamsha
ari ya kudadisi zaidi mambo mbalimbali ya Kiswahili hususani athari za matumizi
ya mitindo mbalimbali katika lugha ya kiswahili. Pia utafiti huu utasaidia
wanafunzi mbalimbali katika kutumia kama rejea za tafiti zao.
Vilevile
utasaidia kuonesha/kuelewa jinsi lugha ya Kiswahili inavyopitia matatizo mengi
katika kupiga hatua zake za kuwa lugha ya kimataifa na masiala mbalimbali
yanayozuia Kiswahili kukua haraka kama lugha zingine za kimataifa.
1.8
Nadharia
1.8.1
Nadharia ya Utabia
Msingi wa utafiti huu kinadharia,
utaegemea dhana ya Nadharia Ya Utabia.Nadharia hii
ilitumika Marekani kati ya 1950-1960. Ina misingi yake katika nadharia ya
kisaikolojia ya utabia.Katika saikolojia, waaasisi wa utabia walilenga kueleza
namna tabia inavyojengwa. Waliamini kuwa tabia ilijengwa tu ikiwa itarudiwa na
kutunzwa. Tabia isiyorudiwa hufifia.
Waliamini kuwa jambo analofunzwa mtu mwanzo linaathiri
lile analojifunza baadaye.Kutokana na maoni hayo, tunafahamu kuwa ujifunzaji wa
lugha ya pili ni sawa na ujifunzaji wa tabia yoyote ile kama vile kukimbia.
Nadharia hii inamsaidia mtafiti kuchunguza kiwango cha madhara ya mtumiaji wa
lugha ya Kiswahili kutokana na mazoea ya kutumia rejesta.
Waasisi
wa lugha hii wanasisitiza yafuatayo:
·
Kukariri
na kurudiarudia matamshi mazuri ya vipande vya mazungumzo hukuza lugha hiyo.
·
Kutofanya
makosa ya kisarufi ili kujenga tabia ya matumizi ya lugha kwa ufasaha.
·
Vipengele
vya lugha hufundishwa kwa njia ya kusikiliza na kuzungumza kasha maandishi huja
baadaye.
·
Miundo
ya kisarufi ya lugha ifundishwe kupitia ukariri wa makala kama tamthiliya.
·
Katika
ufundishaji wa sarufi, wanafunzi wakariri na kuiga vipengele hivi ili wazoee na
baadaye wang’amue wenyewe kwa kukisia kanuni zinazotawala lugha. Kwa mfano,
kurudia umoja na wingi wa nomino za ngeli fulani na baadaye kupewa nomino
katika umoja watambue wingi wake.
Hivyo waasisi wa nadharia hii walichunguza jinsi mtu
anavyojifunza lugha kutokana na mazoea.Hivyo nadharia hii ilimsaidia mtafiti katika
kuchunguza jinsi mazoea ya matumizi ya geuza maumbo yanavyoathiri Kiwango cha
uelewa na ufasaha wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa watumizi wake
kimawasiliano na hata kimaandishi.
Nadharia hii inamsaidia mtafiti kufahamu jinsi mazoea
katika matumizi ya geuza maumbo au lugha yoyote ile yanavyoathiri kiwango cha
umilisi wa lugha ya kwanza au Kiswahili. Matumizi ya geuza maumbo husababisha
kudidimia kwa ubora wa mtumiaji wa
Kiswahili katita viwango vya sarufi na kuogeza makosa ya kisarufi katika viwango
vyote vinne ambavyo ni maumbo, maana, matamshi na muundo wa uandishi. Pia
mazoea ya kuzungumza geuza maumbo huchangia kudidimia kwa msamiati wa lugha ya
Kiswahili kwa watumiaji wake.
Kwa wale ambao wanajifunza lugha ya kwanza ambayo ni
Kiswahili kwao wataathirika sana na lugha ya geuza maumbo kutokana na kuwepo
kwa mazingira ambayo watu wengine wanatumia lugha ya geuza maumbo. Jambo hili
litachangia yeye kujifunza lugha ya Kiswahili iliyojaa kasoro za kisarufi,
kimantiki na isiyo sanifu.
1.8.2 Nadharia ya
umaanishaji
Nadharia nyingine itakayofaa katika utafiti mzima ni ile ya Umaanishaji iliyoasisiwa na Grice (1975). Nadharia hii inaelezea kwamba kuwa watu huwa hawasemi mambo waziwazi; na
ili kupata ujumbe kamilifu kutokana na kile wakisemacho, ni sharti kuwe na
umaanishaji katika maana. Kauli hii imejengwa kwa msingi kuwa wasemaji
humaanisha mambo yanayozidi walichokisema na la muhimu katika kujifunza lugha
ni mawasiliano.
Kwa jumla, nadharia hii inashikilia dhana kuwa maana ya jambo, matukio au
hali fulani hutokana na tafsiri ya kimuktadha pamoja na elimu shirikishi.
Yaani, maana ni zao la ushirikiano baina ya msikilizaji na msemaji kwa
kuzingatia kaida nne: kanuni ya idadi, namna, uhusiano, na ukweli. Nadharia hii
inatusaidia kufahamu kuwa jambo la muhimu katika lugha fulani ni maana ya
maneno yanayotumika.Ikiwa lugha ya geuza maumbo itaendelea kutumika, kiwango
cha ulewa katika mawasiliano kitadidimia kwa kuwa si watu waote wanaotumia
lugha ya Kiswahili wanaelewa maana ya maneno yanayotumiwa katika lugha ya geuza
maumbo.
Nadharia hii inatuonyesha jinsi umuhimu wa maana katika matumizi ya lugha
ulivyo na nguvu kupiku maneno yenyenyewe. Geuza maumbo imechangia kubadilika
kwa maana ya maneno ya Kiswahili na kupewa maana nyingine ambayo watumizi wa
Kiswahili hawafahamu. Jambo hili limechangia kupotoka kwa maana ya maneno ya
Kiswahili na kudidimia kwa kiwango cha hadhi ya Kiswahili kwa kuwa watumizi
wake wamelazimika kuelewa maana fiche ya maneno ya Kiswahili kama jinsi maneno
hayo yanavyomanisha katika lugha ya geuza maumbo.
1.9 Changamoto za Utafiti
Upungufu
wa rejea na muda kutokuwa wa kutosha ni changamoto mojawapo utakaoukabili
utafiti huu. Si hivyo tu, vilevile upungufu wa fedha, kutokupata ushirikiano
kwa baadhi ya watafitiwa.
SURA YA PILI
2.0 Mapitio ya Vitabu
Ili kuweza kujua madhara ya rejesta katika lugha ya
Kiswahili, mtafiti asome makala na vitabu vilivyoandikwa na wataalamu
mbalimbali wa lugha kama inavyooneshwa katika sura hii;
Matumizi ya lugha kwa maana nyingine iliyo finyu, ni Rejesta.
Rejesta ni mtindo wa lugha inayotumika mahali penye shughuli fulani ambayo ni
tofauti na lugha ya kawaida. Kwa mfano, lugh ya wavuvi, washairi, ya
kibiashara, ya kihuni, n.k. Kwa upande mwingine kuna rejesta zinazotokana na
umri, kwa mfano vijana wana rejesta yao, wazee wana yao, wanawake wana yao,
marafiki nao wana rejesta yao, rejesta ya mitaani, nk.
Rejesta:
Halliday (1989), anafasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi au
shughuli. Vilevile fasili hii inaendana na fasili ya Habwe na Karanja (2007).
Kwa ujumla tunaweza kufasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi
fulani, muktadha wa matumizi, lengo na uhusiano wa wanaowasiliana. Katika
muktadha rasmi rejesta hurejelea upande mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi,
adabu maalum na matumizi ya lugha fasaha, mfano katika elimu, mahakamani
nakadhalika. Pia Rejista ni
matumizi ya lugha
kulingana na muktadha maalum. Miktadha tofauti husababisha aina mbalimbali za
lugha. Baadhi ya vipengele vya miktadha hiyo ni mada, eneo la matumizi ya
lugha, mahusiano baina ya wahusika, umri, jinsia, wakati, na kadhalika, mifano
ya rejesta katika lugha ni Mifano ya rejista za lugha ni: lugha ya
mazungumzo,
lugha ya sheria,
lugha ya biashara,
lugha ya sayansi,
na lugha ya dini Massamba, (2004).
Rejesta,
Kwa ujumla tunaweza kufasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi
fulani, muktadha wa matumizi, lengo na uhusiano wa wanaowasiliana. Katika
muktadha rasmi rejesta hurejelea upande mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi,
adabu maalum na matumizi ya lugha fasaha, mfano katika elimu, mahakamani na
kadhalika lengo kubwa huwa ni kutambulisha jamii husika. Kutokana fasihili
imepelekea kuwepo kwa aina mbalimbali za rejesta kama rejesta za mitaani,
rejesta za mahali na rejesta zinazohusu watu. Buliba, Aswani, Kimani Njogu & Alice Mwihaki, (2006)
2.1
Pengo la Utafiti.
Kutokana na mapitio hayo ya tafiti mbalimbali mtafiti ameona
kwamba tafiti nyingi zimeelezea kuhusu kuchipuka na kukua kwa rejesta , lakini
kati ya tafiti hizo hakuna tafiti zozote zilizoelezea kuhusu namna ya matumizi
ya rejesta hususani zinazo wahusu watu katika kipengele cha kugeuza maumbo ya
maneno kinavyo didimiza na kuathiri lugha
ya Kiswahili. Hivyo basi, utafiti huu utakusudia kuziba pengo hilo.
SURA
YA TATU
3.0 Mbinu za Utafiti
Katika utafiti huu mtafiti atatumia mbinu mbalimbali
ambazo zitamwezesha kukusanya data anazozihitaji katika utafiti wake. Mbinu
hizo ni kama vile;
3.1
Hojaji.
Mtafiti ataitumia mbinu hii ili kuweza kupata data
mbalimbali zilizohusu matumizi ya lugha ya geuza maumbo. Baadhi ya maswali
mtafiti atakayouliza yatakuwa kama ifuatavyo;
(i)
Je
wanaifahamu rejesta ya geuza maumbo
(kinyume)?
(ii)
Je
wanatumia rejesta ya geuza maumbo (kinyume) kwa dhamira gani katika
mawasiliano?
(iii) Je wanapendelea lugha ipi baina ya geuza maumbo (kinyume)
na Kiswaahili inayofanikisha mawasiliano haraka?
(iv) Je dhamira zinazopatikana katika matumizi ya geuza maumbo
(kinyume) ni tofauti na zile zinazopatikana katika matumizi ya lugha ya
Kiswahili?
(v)
Wanahisi
matatizo yoyote yale kwa kuwepo kwa lugha ya geuza maumbo (kinyume)?
3.2 Mahojiano.
Mtafiti
atawahoji watu mbalimbali kuhusu uelewa wao wa rejesta ya geuza maumbo
(kinyume) pamoja na Kiswahili na kuwaomba wachangie maoni yao kuhusu ikiwa yapo
matatizo yanayotokana na kuongezeka kwa matumizi ya rejesta ya geuza maumbo
(kinyume) kwa lugha ya Kiswahili. Pia atawaomba wahojiwa waweze kujieleza kwa
Kiswahili sanifu kwa mda mfupi na walinganishe mazungumzo yao ya sasa na yale
ya kabla ya wao kujifunza rejesta ya geuza maumbo (kinyume).
3.3 Kushiriki.
Mtafiti
atashiriki mazungumzo baina yake na watu wa umri mbalimbali katika maeneo yao ya kazi kwa kutumia lugha ya
Kiswahili kama lugha kuu ya mawasiliano. Pia atashiriki katika soga za watu
mbalimbali wanaotumia rejesta ya geuza maumbo.
3.1 Eneo la utafiti
Mtafiti
atafanya utafiti wake katika eneo la Manispaa ya Iringa katika mkoa wa Iringa.
3.2
Zana za Utafiti za Kukusanya Data
Mtafiti atatumia vifaa kama vile kalamu na karatasi katika
kuandika data mbalimbali atakazozipata katika utafiti wake. Pia atatumia:
-
kinasa
sauti.
-
kamera
ya picha tuli.
-
kamera
ya video ili kurekodi mahojiano na majadiliano yote.
Mtafiti atahitajika kusikiliza kwa makini na kuandika
katika karatasi maneno na masuala yatakayojitokeza wakati wa majadiliano baina
yake na watumizi wa lugha ya geuza maumbo na Kiswahili.
3.3
Uteuzi wa Sampuli
Sampuli ya watafitiwa isichaguliwe kiholela bali izingatie
vigezo vifuatavyo; umri na maeneo ya kazi ili kupata wawakilishi sahihi.
Vilevile uteuzi utazingatia umahiri wa wazungumzaji katika kutumia rejesta ya
geuza maumbo (kinyume) na Kiswahili. Ingawa sampuli itazingatia umri, maeneo ya
kazi na umahiri wa lugha, lakini watu wenye umri wa kati wapewa umuhimu mkubwa
kutokana na uzoefu wao wa maisha na kuaminika kwao kuwa wanaujuzi mkubwa wa
lugha husuka, pia kutokana na kutumia mtindo huu kwa muda mrefu inasadikika
kuwa wameshiriki katika matukio mbalimbali na hivyo kuweza kujua vizuri zaidi
dhima na dhamira ya lugha ya Kiswahili. Hivyo basi mtafiti atachagua sampuli ya
takribani watu 122 ambao ni dereva na kondakta wanaofanya shughuli ya kuendesha
magari madogo aina ya haisi na kosta katika Manispaa ya Iringa.
Watafitiwa hawa washiriki katika utafiti wa madhara ya
rejesta ya geuza maumbo (kinyume) katika
lugha ya Kiswahili. Mchango wa sampuli hiyo uwe kama ufuatao; Katika mchanganuo
huo, watu wa rika, Dereva na Kondakta
waonyeshwe kwa kutumia jedwali.
Umri
|
Dereva
|
Kondakta
|
20-24
|
7
|
15
|
25-29
|
30
|
10
|
30-34
|
20
|
10
|
35-39
|
15
|
5
|
40-44
|
10
|
0
|
JUMLA
|
82
|
40
|
3.4
Uchambuzi wa Data
Mtafiti achunguze na kuchambua data alizokusanya ili
ziweze kutumika katika utafiti wake. Ili kupata usahihi katika data mbalimbali
atazokusanya, mtafiti alinganishe na kuzichuja data hizo.
Vilevile kutokana na data atakazozikusanya mtafiti,
vijana wa umri wa miaka 35-49 watakuwa
na ufasaha katika kutumia lugha ya Kiswahili kuliko vijana wa umri wa miaka
20-34 hasa kutokana na madhara finyu ya geuza maumbo kwao ikilinganishwa na
jinsi vijana walivyoadhiriwa na lugha ya geuza maumbo.
Aidha, mtafiti ayagawaanye madhara ya geuza maumbo kwa
lugha ya Kiswahili katika kategoria mbili:
(i)
Umri.
(ii)
Maeneo
ya makaazi.
4.0
Hitimisho
Utafiti huu utahusu madhara ya rejesta katika kudidimia
kwa ufasaha wa lugha ya Kiswahili. Kutokana na uchambuzi wa data, utafiti
utatoa matokeo yanayoonesha kwamba rejesta ina madhara mbalimbali kama vile:
madhara ya kisarufi, madhara ya kimsamiati, madhara ya kiufasaha na umilisi wa
Kiswahili, madhara ya umoja na mshikamano katika jamii.
Kutokana na utafiti huu wa madhara ya rejesta katika
lugha ya Kiswahili yataonekana wazi kuwa matumizi ya rejesta bado yanaendelea
kukiathiri Kiswahili kwa kiwango kikubwa hasa tukirejelea kuwa Kiswahili ni
lugha ya taifa nchini Tanzania. Kiswahili ni lugha inayowapatanisha Watanzania.
Mtindo wa rejesta umeathiri uhusiano uliokuwepo kati ya
madereva, makondakta na abiria kutokana na kuwa abiria wote wanatumia lugha
moja kuu ya Kiswahili inayowaunganisha. Kutokana na kuzuka kwa rejesta hasa ya
kugeuza maumbo (kinyume) baina ya madereva na makondakta, wasioelewa lugha hii
hata kama wanaufahamu mzuri wa Kiswahili wanabanwa nje na wale wanaotumia
mtindo huu wa lugha ya rejesta inayohusisha ugeuzaji wa maneno kwa mfano aribia akiwa na maana ya abiria katika mawasiliano yao.
Lengo kuu la utafiti huu litakuwa kuchunguza suala la
kudidimia kwa kiwango cha ufasaha na ukuaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili
kutokana na matumizi ya rejesta hususani ya kugeuza maumbo (kinyume). Makala
haya yatatoa kauli kwamba matumizi ya rejesta hii inavyoathiri sana matumizi na
hadhi ya lugha ya Kiswahili. Kutokana na mambo
haya yote,utafiti huu unalenga kukusanya data itakayoniwezesha kuratibu,
kuchanganua na kuwasilisha matokeo ya athari ya matumizi ya rejesta katika
lugha ya Kiswahili.
MAREJELEO
Buliba,
Aswani, Kimani Njogu & Alice
Mwihaki. (2006). "Isimujamii kwa Wanafunzi wa Kiswahili", Nairobi:
The Jomo Kenyatta Foundation
Halliday M.A.K (1989). Spoken and written
language.UK: Oxford university press.
Massamba, D. (2004), "Kamusi ya Isimu na Falsafa ya
Lugha. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Nkwera, Fr. F. V.
(2003), Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu, Sekondari na Vyuo.
Creative Prints Ltd: Dar es Salaam.
Subscribe to:
Posts (Atom)